MAKALA 004S: Mahitaji na Hatua za Kufuata ili Kupata Hati ya Umiliki

READ THIS ARTICLE IN ENGLISH

UTANGULIZI

Katika makala hii, mahitaji na hatua muhimu zinazohusika katika kupata Hati ya Umiliki ya Kiserikali zinaelezewa.

A: MAHITAJI ILI KUPATA HATI YA UMILIKI

a) Ardhi lazima iwe imepangwa na kupimwa.
b) Uthibitisho wa umiliki wa ardhi.
c) Uthibitisho wa utaifa.
d) Picha za pasipoti.
e) Malipo ya gharama zinazohusiana na Hati ya Umiliki.


Hayo ni mahitaji ya msingi, Kamishna wa Ardhi anaweza kuhitaji taarifa au mahitaji mengine ya ziada. 


a) Ardhi Lazima Iwe Imepangwa na Kupimwa


Hili ni sharti la msingi ambalo likiachwa litasababisha kutoendelea kwa hatua zingine za kupata Hati ya Umiliki. Upangaji na upimaji wa ardhi unaweza kufanywa na mmoja kati ya hawa wafuatao;

i)Serikali
Hapa wahusika ni idara ya upimaji na ramani, na upangaji katika mamlaka husika kama vile Halmashauri ya Manispaa au Wilaya.

ii) Kampuni binafsi za upangaji na upimaji
Ni lazima mipango ya matumizi ya ardhi na ramani zilizoandaliwa na kampuni binafsi zithibitishwe na mamlaka ya upangaji, na upimaji na ramani katika Halmashauri husika ya Manispaa au Wilaya.


b) Uthibitisho wa Uraia


Ni lazima muombaji wa Hati ya Umiliki awe na kitambulisho kinathibitisha uraia wake.
Kitambulisho hicho kinaweza kuwa Kitambulisho cha Taifa, Hati ya Kusafiria, kivuli cha Cheti cha Kuzaliwa,  Leseni ya Udereva, na Kitambulisho cha Mpiga Kura.

Nyakati hizi Kitambulisho cha Taifa kinasisitizwa zaidi kuliko aina zingine za vitambulisho.
Unakumbuka ustahiki wa umiliki ardhi nchini Tanzania katika Makala 003S? Uthibitisho wa uraia unahitajika ili kuthibitisha kama muombaji anastahiki kumiliki ardhi kisheria.

c) Uthibitisho wa Umiliki wa Ardhi


Ni lazima muombaji apeleke nyaraka halali. zinazothibitisha umiliki wa ardhi husika. Nyaraka hizo ni kama vile Mkataba wa Mauziano (ya ardhi), historia ya kiwanja, na nyaraka za urithi.

e) Malipo ya Gharama Zinazohusiana na Hati ya Umiliki


Kupata Hati ya Umiliki kunahusisha gharama mbalimbali. Gharama hizi zinatambulika kisheria, na zinaorodheshwa hapa chini;

- Ada ya Hati
-Ada ya Usajili wa Ardhi
-Kodi ya Ardhi
-Tozo la Mbele
-Ada ya Ramani ya Hati
-Ushuru wa Serikali
-Ada ya Upimaji

Mjadala wa kina kuhusu gharama zinazohusiana na Hati ya Umiliki unapatikana katika Makala 005S.

B: HATUA ZA KUFUATA ILI KUPATA UMILIKI WA ARDHI KWA HATI


a) Kuwasilisha ombi la umiliki
b) Uamuzi wa kugawiwa ardhi
c) Kupewa umiliki wa hati

a) Kuwasilisha Ombi la Umiliki


Maombi ya umiliki wa ardhi hufanyika kwa kujaza fomu ya maombi. Hii ni fomu maalumu inayoitwa “Fomu ya Ardhi Na. 19 (Maombi ya Haki ya Kumiliki Ardhi).”
Fomu hii inapatikana katika ofisi za ardhi kwenye Halmashauri ya Wilaya au Manispaa.
Baada ya kujaza fomu kwa ukamilifu, muombaji ataiwasilisha fomu hiyo kwenye ofisi ya ardhi kwa taratibu nyingine za kiofisi.
Kumbuka kuwa fomu ya maombi itaambatanishwa na mahitaji yaliyotajwa mwanzoni mwa makala hii kadri utakavyopewa maelekezo kutoka ofisi ya ardhi.

b) Uamuzi wa Kugawiwa Ardhi


Katika hatua hii Kamishna wa Ardhi atafanya uamuzi wa kukubali au kukataa maombi ya Hakimiliki. Endapo ataamua kunyima umiliki wa ardhi, atatakiwa kutoa sababu za kufanya hivyo.

c) Kupata Umiliki wa Hati


Hati ya Umiliki itatolewa iwapo Kamishna ataridhika kuwa muombaji wa hati ametimiza masharti, na amefanya uamuzi wa kutoa Hakimiliki.

Je, una swali lolote kuhusu makala hii?
Je, una nyongeza kuhusu kupata Hati ya Umiliki?

Usisite kutuandikia kwenye sehemu ya maoni.

Ahsante na Karibu!
The Aliland Team

Comments

Unknown said…
Keep it up my brother, every things come with reasons.never give up