Umiliki wa Ardhi Kisheria Nchini Tanzania
Utangulizi
Katika makala hii mjadala utahusu aina za Umilikaji Ardhi
nchini Tanzania. Aina hizi ndio zinaunda umiliki wa ardhi kisheria.
Ili kukuza uelewa zaidi wa mada,
makala itajadili vigezo vya kumiliki ardhi na nafasi ya wasio raia wa Tanzania
katika kumiliki ardhi.
Nani Anaweza Kumiliki Ardhi Nchini Tanzania?
Wafuatao wanastahiki kisheria
kumiliki ardhi kupitia aidha Hakimiliki ya Kiserikali au Hakimiliki ya Kimila;
a) Mtu yeyote ambaye ni Mtanzania, mwanamme au
mwanamke.
b) Kikundi cha watu ambao ni raia wa Tanzania walio
katika umoja wa kisheria au la, au ni wabia au washirika.
Ni Ipi Nafasi ya Wasio Raia Katika Kumiliki Ardhi?
Kwa ujumla, sheria za Tanzania
haziruhusu wasio raia kumiliki ardhi isipokuwa kwa lengo la uwekezaji tu.
Sheria ya Ardhi inaeleza kuwa,
“Mtu ambaye sio raia wa
Tanzania, au kikundi cha watu au mtu ambaye ana shirika lenye hisa, ambao wengi
wa wanahisa wake sio Watanzania hawana haki ya moja kwa moja ya kumiliki ardhi
nchini na kupewa hakimiliki ya ardhi isipokuwa tu kama watapewa ardhi hiyo kama
wawekezaji wa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997.”
Aina za Umiliki wa Ardhi
Kuna aina kuu mbili za umiliki wa
Ardhi nchini Tanzania ambazo ni;
a) Hakimiliki ya Kiserikali
b) Hakimiliki ya Kimila
a) Hakimiliki ya Kiserikali
Hii ni hakimiliki inayotolewa na
Rais (kupitia Kamishna wa Ardhi) kwa mtu, taasisi au kikundi cha watu ambayo
huwaruhusu kumiliki ardhi katika Ardhi ya Jumla na Ardhi ya Hifadhi.
Umiliki hukamilika kwa kupatiwa
Hati ya Hakimiliki ya Kiserikali ambayo hutaja masharti ya umiliki huo.
Makala tatu zijazo zitajadili
vipengele mbalimbali vya Hakimiliki ya Kiserikali.
b) Hakimiliki ya Kimila
Hakimiliki ya Kimila hupatiwa
wanakijiji katika Ardhi ya Kijiji, na maana yake ipo katika namna mbili;
Maana ya kwanza inajumuisha ardhi
inayogawiwa na Halmashauri ya Kijiji. Hapa, hakimiliki inaundwa kwa kutoa Hati
ya Hakimiliki ya Kimila.
Maana ya pili hujumuisha ardhi
iliyopatikana chini ya sheria za kimila kupitia, kwa mfano, kununua, kusafisha
pori, kupewa zawadi, na urithi. Hapa, umilikaji ardhi hufuata taratibu za
kimila na desturi za jamii husika.
Comments