Kununua Ardhi Iliyosajiliwa Nchini Tanzania- SEHEMU A

Ni ukweli usiopingika kuwa ardhi ni rasilimali muhimu. Tunaweza kuhitaji kununua ardhi katika kipindi fulani cha maisha yetu kwa ajili ya makazi, biashara, kilimo na kadhalika. Hivyo, kuna umuhimu wa kuelewa vitu vya kuzingatia katika kununua ardhi.

Kanuni kubwa katika ununuzi wa ardhi ni ile isemayo “Mnunuzi na Awe Macho”. Hii inamaanisha kuwa mnunuzi wa ardhi anatakiwa awe makini katika mchakato wote wa kununua. Ardhi imekuwa ni rasilimali yenye migogoro mingi siku hizi.

Ni vyema kufahamu kuwa kuna “ardhi iliyosajiliwa” na “ardhi isiyosajiliwa”
Ardhi iliyosajiliwa ni ile iliyopangwa, kupimwa na kuorodheshwa au kurekodiwa katika daftari maalumu la Serikali (katika ofisi ya Msajili wa Hati). Ardhi isiyosajiliwa ni kinyume cha ardhi iliyosajiliwa.

Katika makala hii tumeelezea hatua na vitu vya msingi vya kuzingatia wakati wa kununua ardhi iliyosajiliwa nchini Tanzania.

Zifuatazo ni hatua kuu za kufuata katika ununuzi wa ardhi iliyosajiliwa;
  1. Uchunguzi wa kina wa kiwanja
  2. Kuandaa na kusaini nyaraka za kisheria
  3. Kufanya malipo kwa muuzaji

HATUA YA KWANZA

UCHUNGUZI WA KINA WA KIWANJA

Katika hatua hii, mnunuzi anatakiwa kuchunguza aina mbili za taarifa;
i) Taarifa za Kisheria
ii)Taarifa za Kimuonekano za Kiwanja
   

i) TAARIFA ZA KISHERIA

Taarifa hizi  zinatumika kufahamu  hali ya kisheria ya kiwanja. Lengo kuu la kufanya uchunguzi wa kisheria ni kujua kama ardhi inamilikiwa kisheria au inafuata matakwa ya kisheria.

Katika kufanya uchunguzi huu, mnunuzi anatakiwa kwanza kuuliza taarifa kutoka kwa muuzaji ,  baada ya hapo atamuomba kivuli  cha Hati ya Umiliki ili kuthibitisha taarifa hizo katika ofisi ya ardhi kwa kuomba “Official Search”.

Mnunuzi anatakiwa kuchunguza taarifa zifuatazo;

a) Mmiliki au Wamiliki wa Kiwanja
Mnunuzi anatakiwa kufanya jitihada za kumfahamu mmiliki halali wa kiwanja kinachouzwa.
Ardhi inaweza kumilikiwa na mtu mmoja, taasisi, au umiliki wa pamoja (kama vile, mali za ndoa au mali za urithi).
Hivyo, kuonekana kwa mmiliki mmoja kusimzuie mnunuzi kuchunguza zaidi juu ya uwepo wa mmiliki mwingine.

b) Historia ya Kiwanja
Ni muhimu mnunuzi kufahamu namna ambayo mmiliki wa sasa (muuzaji) aliipata ardhi hiyo (aidha kwa kupewa zawadi, kununua, kurithi au kugawiwa na Serikali).
Hii ni taarifa muhimu kwa sababu inamsaidia mnunuzi kuelewa vizuri kiwanja anachohitaji kununua na hivyo kupunguza migogoro hapo mbele.

c) Kiwanja kuwekwa Rehani
Mnunuzi anatakiwa amuulize muuzaji kama kiwanja kimewekwa rehani au dhamana  ya mkopo kutoka taasisi za kifedha, na kama tayari mkopo umeshalipwa au la.

d) Ulipaji wa Kodi ya Ardhi
Hapa, mnunuzi anatakiwa kuulizia taarifa za kina kuhusu ulipaji wa kodi ya ardhi.
Kwa mfano, ni kiasi gani cha kodi ya ardhi huwa kinalipwa katika kiwanja husika? Mara ya mwisho kulipa kodi ya ardhi ilikuwa lini? Risiti za ulipaji kodi ya ardhi ziko wapi?

e) Upangishaji wa Ardhi
Muuzaji anaweza kuwa amepangisha ardhi husika na kuamua kutomuambia mnunuzi taarifa hii kwa makusudi.
Ni jukumu la mnunuzi kuchunguza zaidi taarifa kuhusu upangishaji. Itamsaidia kufanya uamuzi wa busara wa kununua au kutonunua, na hatimaye migogogo hapo mbele itaepukwa.

f) Zuio

Zuio ni nyaraka ya kisheria inayozuia  kufanya kitendo chochote katika  kiwanja husika bila kutoa taarifa kwa aliyeweka zuio hilo. Hii inaweza kuwa ni zuio la mahakama  au zuio la mtu mwingine mwenye masilahi katika kiwanja kama vile mke au mume.

Ili kuendelea na taratibu zingine za ununuzi, ni lazima mnunuzi ajiridhishe kuwa kiwanja anachohitaji kununua hakina zuio.


g) Migogoro ya Ardhi
Migogoro ya ardhi imekuwa mingi siku hizi. Migogoro hii inaweza kuwa migogoro ya mipaka, migogoro ya umiliki(kwa mfano, katika mali za ndoa), migogoro ya urithi, migogoro na mamlaka, na kuuza au kugawa kiwanja kimoja zaidi ya mara moja.
Hivyo, mnunuzi anatakiwa kufanya jitihada stahiki katika uchunguzi wa uwepo wa migogoro katika ardhi anayohitaji kununua.

Je, ni taarifa zipi zingine za kisheria anazotakiwa kufahamu mnunuzi kabla ya kununua ardhi? 

Sehemu ya pili ya makala hii tutaelezea taarifa zingine za kisheria, taarifa za kimuonekano wa kiwanja, pamoja na hatua ya pili na ya tatu ya ununuzi wa ardhi.
Tafadhali usikose sehemu ya pili ya makala hii.


Ahsante na karibu sana!
The Aliland Team


Comments