Kununua Ardhi Iliyosajiliwa Nchini Tanzania -SEHEMU B

READ THIS ARTICLE IN ENGLISH


Katika makala hii tutaendelea kuelezea taarifa za kisheria ambazo mnunuzi anapaswa kuzichunguza kabla ya kununua ardhi. Pia taarifa za kimuonekano wa kiwanja, pamoja na hatua ya pili na ya tatu ya ununuzi wa ardhi zitajadiliwa.


h) Mahali kiwanja kilipo
Mnunuzi anatakiwa kuchukulia suala la mahali kiwanja kilipo kwa uzito. Anatakiwa kuepuka kiwanja kilichopo katika maeneo ya hifadhi kama vile hifadhi ya barabara, maeneo ya wazi, chanzo cha maji, hifadhi ya wanyamapori na hifadhi ya misitu, au kiwanja kilichopo katika ardhi ya taasisi ya serikali au kampuni binafsi.

i) Utwaaji wa Ardhi
Baadhi ya maeneo yanaweza kuwa yametwaliwa ili kupisha miradi ya Serikali kama vile ujenzi wa barabara na hospitali.
Mnunuzi anatakiwa kuchunguza taarifa hii, na kuepuka maeneo hayo kama ikifahamika kuwa watu watalipwa au walishalipwa fidia.

j) Uhalisi wa Hati ya Umiliki
Wakati wingine taarifa zilizopo kwenye hati zinaweza kuwa ni sahihi lakini Hati ya Umiliki si halisi. Hii ni kutokana na ukweli kuwa hati feki za umiliki ni jambo linalozidi kutamalaki.
Ni jukumu la mnunuzi kujiridhisha kuhusu uhalisi wa hati.

Kwa kawaida ni vigumu kwa muuzaji kumpatia mnunuzi hati halisi aende kujiridhisha uhalisi wake. Hivyo, mnunuzi amuombe muuzaji waambatane akiwa na hati halisi ili kuthibitisha kama hati ni halisi au la.

TAARIFA ZA KIMUONEKANO ZA KIWANJA

Kuchunguza taarifa za kimuonekano za kiwanja huhusisha kujionea kiwanja kwa macho na kuuliza majirani wa eneo kiwanja kilipo.
Mnunuzi anatakiwa  kutembelea kiwanja na kuchunguza vitu vifuatavyo;

a) Mipaka
Mnunuzi anatakiwa kumuomba muuzaji  amuoneshe mipaka ya kiwanja.
Vile vile, mnunuzi anatakiwa aende mbali zaidi kwa kutembelea kiwanja kwa muda wake mwenyewe na kuchunguza mawe ya mipaka na pia kuwauliza majirani.

b) Aina ya udongo,  topografia, ukubwa na umbo la kiwanja
Mnunuzi anatakiwa kufanya jitihada ya kuelewa aina ya udongo, ardhi yenye miinuko au tambarare, ukubwa na umbo la kiwanja. Kisha baada ya hapo afanye maamuzi kama kinafaa kwa matumizi anayokusudia, kama vile makazi na kilimo.

c) Huduma za Kijamii
Ndugu msomaji, chukulia tu anahitaji kununua ardhi kwa ajili ya makazi, biashara au kilimo. Je, si busara kuchunguza upatikanaji wa barabara, umeme, maji, masoko, shule au huduma za kiimani katika eneo  analotaka kununua kiwanja?

Hivyo, kabla ya kununua kiwanja, ni muhimu mnunuzi kuchunguza huduma za kijamii zinazopatikana katika eneo kiwanja kilipo.

d) Hali ya Kijiografia ya eneo
Usalama ni jambo muhimu, hivyo mnunuzi anatakiwa kuchunguza vizuri ili kuepuka maeneo ambayo yanaathiriwa kirahisi na mmomonyoko wa ardhi, mafuriko na vimbunga. Anatakiwa kuuliza kwa muuzaji au majirani, na kutafuta taarifa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali juu ya hali ya kijiografia ya eneo kiwanja kilipo.


HATUA YA PILI

KUANDAA NA KUSAINI NYARAKA ZA KISHERIA


Hatua hii ya pili inahusisha shughuli zifuatazo;

i) Kuafikiana kwenye masharti ya mauziano. Kwa mfano, iwapo malipo yafanyike kwa fedha taslimu au kwa njia ya benki, na iwapo ni malipo ya awamu kwa awamu au fedha yote kwa pamoja. 

ii) Kuandaa Mkataba wa Mauziano chini ya wakili.

iii) Kusaini Mkataba wa Mauziano ambao utasainiwa na muuzaji, mnunuzi na mwanasheria, kisha baada ya hapo wakili atagonga muhuri.

Nyaraka zingine muhimu za kisheria zinazohusika katika kununua ardhi ni;

 i) Fomu Na. 29 ambayo itasainiwa na muuzaji.

ii Fomu Na. 30 ambayo itasainiwa na muuzaji.

iii) Fomu Na. 35 ambayo itasainiwa na muuzaji na mnunuzi.

iv) Ridhaa ya Mwanandoa, ambayo ni nyaraka inayosainiwa na mume/mke wa muuzaji kama ardhi inayouzwa ni mali ya ndoa.

v) Ridhaa ya Warithi, ambayo huhusisha saini za warithi wote halali wa mali za marehemu na msimamizi wa mirathi kama ardhi ni mali ya urithi.

HATUA YA TATU


KUFANYA MALIPO KWA MUUZAJI


Hatua hii ya mwisho inahusisha kufanya malipo kulingana na makubaliano yaliyofanyika kati ya mnunuzi na muuzaji. Kwa mfano, malipo kwa fedha taslimu au kwa njia ya benki, na iwapo ni malipo ya awamu kwa awamu au fedha yote kwa pamoja.
Inashauriwa fedha zilipwe kwa njia ya benki ilikaratasi za muamala ziwe ushahidi wa malipo.

BEI YA KIWANJA?
Bei ni suala nyeti sana katika ununuzi wa ardhi, na hivyo mnunuzi anatakiwa kuafikiana na muuzaji kuhusu bei mapema iwezekanavyo kabla ya kuanza kufanya uchunguzi wote uliojadiliwa katika hatua ya kwanza.



Ahsante na karibu sana!

The Aliland Team

Comments