MAKALA 006S: Masharti katika Hati ya Umiliki

READ THIS ARTICLE IN ENGLISH

UTANGULIZI 


Baada ya kufanikiwa kupata Hati ya Umiliki inashauriwa kuisoma na kuielewa vizuri.

Miongoni mwa vitu vinavyopatikana katika Hati ya Umiliki ni masharti ya Hakimiliki ya ardhi.


Katika Makala hii mjadala utakuwa kuhusu masharti yanayopatikana katika Hati ya Umiliki ambayo mmiliki wa ardhi anatakiwa kuyafuata ama kuyatimiza.





Masharti hayo yanaelezwa hapa chini;

i) Kulipa Kodi ya Ardhi

Mmilki anatakiwa kulipa Kodi ya Ardhi kila mwaka katika kipindi chote cha umiliki. Kodi ya Ardhi  inaweza kubadilishwa na Kamishna wa Ardhi katika vipindi tofauti.
Kwa nini tunalipa Kodi ya Ardhi?
Ni kwa namna gani mmiliki anaweza kufahamu kiasi cha Kodi ya Ardhi anachotakiwa kulipa katika mwaka husika?
Ni kwa namna gani mmiliki anaweza kulipia Kodi yake ya Ardhi?
Hapa tumechochea tu uelewa wa mwanzo kuhusu Kodi ya Ardhi
Tutakuwa na mjadala wa kina kuhusu Kodi ya Ardhi katika moja ya makala za wiki zijazo.

ii) Kulinda Mawe ya Mipaka

Mmiliki wa ardhi anapaswa kulinda mawe yote ya mipaka yaliyopo katika ardhi yake katika kipindi chote cha Hakimilki.
Mawe ya mipaka huwekwa kipindi cha upimaji wa ardhi na husaidia kutenganisha ardhi zinazopakana.
Ikitokea mawe ya mipaka yanakosekana katika ardhi, mmiliki anatakiwa kuyarejesha au kuweka tena mawe hayo kwa kutumia gharama zake.

iii) Kutunza Mazingira

Mmiliki anatakiwa kulinda na kutunza mazingira. Hii inajumuisha kulinda ardhi yake dhidi ya mmomonyoko wa udongo.

iv) Masharti ya Ujenzi

Masharti ya ujenzi yaliyomo ndani ya Hati ya Umiliki ni haya yafuatayo;
a) Jengo liwe katika vifaa vya kudumu vya ujenzi.

b) Kuwasilisha ramani ya jengo katika mamlaka husika ndani ya miezi sita (6) baada ya kuanza kwa muda wa Hati Miliki.

c) Ujenzi wa (ma)jengo uanze ndani ya miezi sita (6) baada ya kuthibitishwa kwa ramani ya jengo.

d) Ujenzi ukamilike ndani ya miezi thelathini na sita (36) toka kuanza kwa muda wa Hati Miliki.

e) Sharti la nini kiwepo juu ya ardhi. Kwa mfano, nyumba moja tu na mabanda ya kawaida na muhimu.

v) Matumizi ya Ardhi

Hati ya Umiliki hutoa masharti ya matumizi ya ardhi husika. Mmiliki anatakiwa afuate maelekezo yaliyooneshwa katika Hati kuhusu matumizi ya ardhi yake. Kutofuata maelekezo hayo kunaweza kupelekea kuchukuliwa hatua za kisheria kama vile amri ya kusimamisha ujenzi au kubomoa jengo.
Ikiwa mmiliki anahitaji kubadilisha matumizi ya Hakimilki yake, anatakiwa kufuata taratibu zilizowekwa za kubadilisha matumizi.

vi) Uthibitisho wa Kutoa Haki ya Umiliki kwa Kamishna wa Ardhi

Mmiliki haruhusiwi kutoa Haki yake ya Umiliki kwa mtu mwingine ndani ya miaka mitatu baada ya kuanza kwa muda wa Hati Miliki bila ya ithibati ya Kamishna wa Ardhi

vii) Kutoa Taarifa ya Miamala ya Ardhi kwa Kamishna wa Ardhi

Ni lazima taarifa iwe katika fomu maalumu na itolewe kabla au wakati muamala unafanyika. Pia iambatanishwe na tozo na kodi zinazohusiana na muamala huo.

viii) Kufuta Hati ya Umiliki

Nchini Tanzania, mamlaka ya mwisho ya umiliki wa ardhi yamekabidhiwa kwa Raisi (Hati ya Hatima). Hivyo, Rais anaweza kufuta Hati ya Umiliki kwa nia njema au manufaa ya umma.


Unataka kujifunza zaidi? 
Tazama video hii inayoelezea masharti ya umiliki wa ardhi.



Ahsante na karibu sana!
The Aliland Team

Comments