Njia za Kupata Ardhi Nchini Tanzania

Utangulizi
Nchini Tanzania, kila mwanajamii ana haki sawa ya kupata ardhi. Makala hii inaelezea njia mbalimbali ambazo mtu au taasisi anaweza kupata ardhi. Kwa kuelewa njia hizi tunaamini utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupata, na baadaye kumiliki, ardhi. Njia hizi ni;
a) Kugawiwa na Serikali              
b) Kununua                  
c) Urithi
d) Kupewa Zawadi                       
e) Upangishaji  
f) Kusafisha pori lisilomilikiwa /lisilokaliwa na mtu

READ THIS ARTICLE IN ENGLISH

a) Kugawiwa na Serikali

Njia hii huhusisha kugawiwa ardhi na mamlaka husika ya Serikali. Mtu huomba kugawiwa ardhi ardhi kwa kujaza fomu maalumu.
Ardhi ya Kijiji hugawiwa na Halmashauri ya kijiji kwa idhini ya Mkutano Mkuu wa kijiji (Mkutano wa wanakijiji wote walio na umri wa miaka 18 na kuendelea).
Ardhi ya Hifadhi hutengwa na Wizara ya ardhi kwa kushirikiana na mamlaka za hifadhi husika.
Ugawaji wa Ardhi ya Jumla hufanywa na Halmashauri ya Wilaya na Manispaa kwa waombaji wa maeneo hayo.

b) Kununua

Sheria inatoa ruhusa ya kununua ardhi kwa mtu au taasisi yenye uwezo wakati mmiliki anapotaka kuuza ardhi yake. Ardhi inaweza kuwa ya Kijiji, Hifadhi au Jumla.
Tutaijadili kwa kina njia hii katika wiki zijazo.
BOFYA HAPA KUSOMA KUHUSU KUNUNUA ARDHI

c) Urithi

Mtu anaweza kupata ardhi kwa njia ya kurithi kutoka kwa wazazi, au mume (kwa wanawake)
Njia hii inaweza kutazamwa katika mitazamo miwili; uwepo wa wosia wa marehemu, na kusipokuwepo wosia wa marehemu.
Pale wosia unapokuwepo, warithi waliotajwa katika wosia watarithi mali za marehemu ikiwemo ardhi.
Pale wosia usipokuwepo, Msimamizi wa Mirathi anachaguliwa na mali za marehemu zinagawanywa kwa kutumia Sheria ya Serikali.
Katika namna zote mbili hapo juu, wanawake wana haki sawa na wanaume kwa njia ya urithi.

d) Kupewa Zawadi

Mtu au taasisi inaweza kupewa ardhi na rafiki, ndugu au mtu yeyote kama zawadi, na hiyo inakuwa njia mojawapo ya kupata haki ya ardhi.
Mtu aliyeandika wosia ana uhuru wa kutoa zawadi ya baadhi ya mali zake au mali zote kabla ya kifo kwa kuangalia upendo unaotokana na kuwepo kwa undugu wa damu.Ikiwa anayetoa ardhi kama zawadi yupo katika ndoa, basi ni lazima mume/mke wake aridhie kuhamisha/kuhawilisha ardhi ambayo ni mali ya ndoa

e) Upangishaji

Njia hii huhusisha kupata haki ya kutumia ardhi kwa muda maalumu uliokubaliwa, ikifuatiwa na malipo ya kodi (pango) kwa mmiliki wa ardhi.
Tofauti kati ya Upangishaji na njia nyingine za upatikanaji wa ardhi ni kuwa upangishaji unakupatia haki pungufu na yule anayekupangisha.
Wanaume, wanawake na taasisi wana haki sawa ya kupata ardhi kupitia njia hii.

f) Kusafisha pori lisilomilikiwa /lisilokaliwa na mtu

Hii ni njia kongwe ya kupata ardhi nchini Tanzania ambapo mtu huingia katika eneo kama vile pori na kusafisha kisha kuliweka katika matumizi. Pori linalosafishwa linaweza kuwa Ardhi ya Kijiji, Hifadhi, au ya Jumla.
Ni ngumu kutumia njia hii nyakati hizi, lakini bado inatumika katika maeneo mengi ya Tanzania.
Pale ambapo utatakiwa na mamlaka kufuata taratibu kama vile kusajili ardhi, utatakiwa kutii amri hiyo.
Pia, kama utatakiwa kuhama eneo hilo basi mamlaka husika itatakiwa kulipa fidia ya maendelezo uliyoyafanya katika ardhi hiyo.

Hitimisho

Ifahamike kuwa kupata ardhi peke yake si mwisho, na sio uthibitisho wa umiliki. Inatakiwa kumiliki ardhi kisheria ili kuhakikisha usalama wa milki.

Somo kuhusu umiliki wa ardhi kisheria litajadiliwa kwenye makala Makala 003S.


Comments