Maana ya Ardhi na Mgawanyo wa Ardhi Nchini Tanzania

SEHEMU A

Maana ya Ardhi

Kuna tafsiri kadhaa za ardhi ambazo zimetolewa na makundi mbalimbali kama vile dini, wanajiografia na wanauchumi.
Hata hivyo, inafaa zaidi kutumia tafsiri iliyotolewa na Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 ambayo inatafsiri kuwa;
"Ardhi" ni ile inayojumuisha vitu vyote vilivyo juu na chini ya uso wa nchi vikiwemo majengo, uoto wa asili na maendelezo yote yaliyofanywa isipokuwa madini na bidhaa za mafuta na gesi"
Pengine utakuwa umegundua kuwa moja ya sifa ya msingi ya tafsiri ya hapo juu ni kutojumuishwa kwa madini na bidhaa za mafuta na gesi katika ardhi.

Kwa nini petroli na aina zote za madini zinazopatikana chini ya ardhi sio sehemu ya ardhi?
Serikali ya Tanzania imefanya hivyo ili kuwezesha matumizi na umiliki wa pamoja kitaifa na kunufaisha umma wa watanzania kwa sababu ardhi ni maliasili haba. 

READ THIS ARTICLE IN ENGLISH



SEHEMU B

Makundi ya Ardhi Nchini Tanzania


Kulingana na Kifungu 4(4) cha Sheria Na.4 ya Ardhi, ardhi ya Tanzania imegawanywa katika makundi yafuatayo;
a) Ardhi ya Hifadhi
b) Ardhi ya Kijiji
c) Ardhi ya Jumla

Ni Nini Lengo la Mgawanyo Huu?

Lengo ni kuwezesha usimamizi wa ardhi chini ya Sheria Na.4 ya Ardhi ya mwaka 1999 na sheria zote zinazohusiana na ardhi.

Makundi ya ardhi yanaelezewa hapa chini;

a) Ardhi ya Hifadhi


Ardhi ya Hifadhi ni ardhi inayolindwa kisheria, au ardhi iliyotengwa au kuhifadhiwa kwa matumizi maalumu ya kitaifa au kijamii kwa manufaa ya raia au wanajamii wote.

Ardhi hii hujumuisha; hifadhi za taifa; ardhi ilihifadhiwa kwa huduma za umma; hifadhi za misitu; hifadhi za maji; hifadhi za barabara;
hifadhi za maeneo ya wazi; hifadhi za wanyamapori; na ardhi ambazo kama zikifanyiwa maendelezo zitaleta hatari kwa mazingira, kwa mfano, kingo za mto. Ardhi ya Hifadhi ni asilimia 28 ya ardhi yote nchini Tanzania.


Kundi hili liko chini ya usimamizi wa sheria na mamlaka mbalimbali kutegemeana na aina ya hifadhi. Mfano, ardhi ya hifadhi za mbuga za wanyama iko chini ya usimamizi wa Sheria ya Mbuga za Wanyama ya mwaka 2009 na chombo chenye mamlaka ya kusimamia mbuga za wanyama ni Shirika la Hifadhi za Taifa la Wanyama (TANAPA).

b) Ardhi ya Kijiji

Hii ni ardhi iliyo ndani ya kijiji kilichosajiliwa na kubainishwa mipaka, na ile iliyokubalika na Halmashauri ya Kijiji husika kuwa ni ardhi ya kijiji; na ardhi ambayo si ya hifadhi, na kwa muda wa miaka kumi na miwili au zaidi kabla ya Sheria ya Ardhi ya Kijiji Na.5 kutungwa, wanakijiji wamekuwa wanaikalia na kuitumia kama ardhi ya kijiji na pasipo kuwepo na aina yoyote ya umiliki au matumizi kabla au wakati  kipindi hicho. Ardhi ya kijiji inachukua asilimia 70 ya ardhi yote nchini Tanzania.

Kundi hili la ardhi lipo chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Kijiji, Kamati ya Maamuzi ya Kijiji, Mkutano Mkuu wa Kijiji, Halmashauri ya Wilaya, na Kamishina wa Ardhi.

c) Ardhi ya Jumla

Sheria ya Ardhi inatafsiri Ardhi ya Jumla kuwa ni ardhi yote ya umma inayobaki baada ya kuondoa ardhi ya kijiji na ardhi ya hifadhi, na inajumuisha ardhi ya kijiji ambayo haikaliwi wala kutumiwa na wanaKijiji. Hivyo, Ardhi ya Jumla hujumuisha mapori, ardhi ya miji, majiji na halmashauri, ambayo hayajatengwa kwa matumizi ya umma.
Ardhi ya Jumla, kulingana na Sheria ya Ardhi ya Kijiji, ni ardhi yote ya umma inayobaki baada ya kuondoa ardhi ya kijiji na ardhi ya hifadhi. Tafsiri hii haijumuishi ardhi ya kijiji ambayo haikaliwi wala kutumiwa na wanaKijiji. Hivyo, kuna mkanganyiko wa Sheria ya Ardhi na Sheria ya Ardhi ya Kijiji katika kutafsiri Ardhi ya Jumla.
Ardhi ya Jumla ipo chini ya usimamizi wa Kamishna wa Ardhi.

Hitimisho

Ardhi ya Jumla na Ardhi ya Hifadhi zinasimamiwa na Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999, ilhali Ardhi ya Kijiji inasimamiwa na Sheria ya Ardhi ya Kijiji Na. 5 ya mwaka 1999.

Kuna hitaji la kusawazisha tafsiri ya “Ardhi ya Jumla” katika Sheria ya Ardhi na Sheria ya Ardhi ya Kijiji ili kuondoa mkanganyiko uliopo.


Inawezekana kuhawilisha aina moja ya Ardhi kwenda kwenye aina nyingine. Uwezekano huu upo wa namna mbili kisheria;

i) Uhawilishaji wa Ardhi ya Kijiji kuwa Ardhi ya kawaida au Ardhi ya Hifadhi
ii) Uhawilishaji wa Ardhi ya kawaida au Ardhi ya Hifadhi kuwa Ardhi ya Kijiji.


Ahsante na Karibu Sana!
The Aliland Team

Comments